
30/07/2025
Katika tukio la kusikitisha lililotokea nchini Marekani, Jaysen Carr (12) amefariki dunia baada ya kuambukizwa na vimelea hatari vya Naegleria fowleri, vinavyojulikana k**a (Amiba mla Ubongo) baada ya kuogelea katika ziwa la 'Lake Murray', South Carolina.
Amiba (Amoeba) hawa hupatikana kwa wingi katika maji ya asili yenye joto, na hushambulia Ubongo kwa kasi kubwa na mara nyingi husababisha kifo siku chache baada ya dalili kuanza.
Amiba hawa hawawezi kuonekana kwa macho wala kugunduliwa kwa urahisi na waogeleaji. Wakati wa kiangazi ambapo joto hupanda na kiwango cha maji kinashuka, viwango vyake huongezeka, na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi kwa watu wanaoingia majini hususan kupitia Pua.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), maambukizi yake ni nadra sana kutokea lakini yana kiwango cha vifo kinachofikia 97%
Kujikinga dhidi ya Amiba hii hatari inashauriwa kuepuka kuruhusu maji ya asili kuingia puani wakati wa kuogelea, kutumia 'Nose clips', au kuogelea katika maji safi ya mabwawa yanayosafishwa. Pia ni muhimu kuepuka kuruka kwa kichwa katika maji ya asili yenye Joto, na kuhakikisha kuwa maji ya kutumia kwenye matibabu ya Pua ni yaliyochemshwa au yaliyo na Chumvi maalum (Saline).