06/01/2026
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo amezindua rasmi Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya saratani ocean road, katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Taasisi hiyo.
Akizungumza na wajumbe wa bodi hiyo, mwenyekiti pamoja na menejiment, Mhe. Mchengerwa amewataka kudumisha mshikamano baina yao katika kutekeleza majukumu ya Bodi pamoja kupeana mawazo yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la Taasisi hiyo.
Mhe.Mchengerwa ameipongeza bodi iliyomaliza muda wake pamoja na menejimenti ya Taasisi hiyo kwa kutekeleza yale yaliyoazimiwa katika Kipindi kilichopita, huku akitoa pongezi za kipekee kwa Mwenyekiti wa bodi Prof. Ephata Kaaya kwa kuteuliwa tena na Raisi kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya Taasisi ya saratani ocean road.
Aidha Mhe. Mchengerwa amejionea uwekezaji uliofanyika katika Taasisi hiyo zikiwemo mashine mbalimbali zilizopo za uchunguzi na matibabu ya saratani zilizosimikwa katika kipindi kilichoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, huku akitoa pongezi za dhati za usimamizi madhubuti unaofanywa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Diwani Msemo katika kuboresha Taasisi ya saratani ocean road.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi Prof. Ephata Kaaya amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuja kuzindua Bodi hiyo huku akiahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na waziri pamoja na kufanya ubunifu mbalimbali katika kuboresha huduma zaidi za Taasisi ili iweze kusonga mbele kwa kasi ya serikali ya awamu ya sita.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya saratani ocean road Dkt. Diwani Msemo amesema kuwa kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali katika ununuzi wa mashine nyingine za tiba mionzi itapelekea kupunguza muda wa kusubiri kwa matibabu hayo kutoka wiki ishirini mpaka wiki mbili, kwani kwa sasa mashine zitakuwa za kutosha, hivyo itaboresha utoaji wa huduma hiyo.