31/12/2025
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kinondoni/Ubungo wametoa mafunzo maalumu kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Temeke kuhusu mbinu salama za kushughulikia matukio yanayohusisha nyuki.
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na B.O Nathanael Nuru kutoka TFS yamehusisha jumla ya Maafisa 8 na Askari 31 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Warsha hiyo imefanyika katika Ofisi ya Jeshi la Zimamoto Temeke, ikiwa na lengo la kuongeza uwezo wa watendaji kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la matukio ya nyuki katika maeneo ya mijini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Nathanael alisema kwamba kumekuwa na ongezeko la malalamiko ya wananchi kuhusu makundi ya nyuki kuingia katika makazi, Ofisi za umma, mashuleni, viwandani na maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu, jambo linalohitaji wataalamu wenye ujuzi wa kitaalamu na tahadhari za kiusalama.
Alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo washiriki katika kutoa huduma ya kwanza kwa wahanga wa mashambulizi ya nyuki, pamoja na kutumia mbinu salama za kuwaondoa nyuki waliopotea au kujenga viota katika maeneo yasiyoruhusiwa bila kuhatarisha maisha ya watu.
Aidha, TFS imesisitiza kuwa kuongeza uelewa wa vikosi vya uokoaji kuhusu tabia za nyuki na njia bora za kushughulikia matukio yanayowahusisha ni hatua muhimu katika kulinda usalama wa wananchi na kuhifadhi viumbe hao wenye mchango mkubwa katika uchavushaji na uhifadhi wa mazingira.