15/04/2026
HOSPITALI YA AMANA YAKABIDHIWA MSAADA WA JENGO MAALUM LA HUDUMA RAFIKI KWA VIJANA
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana imekabidhiwa msaada wa jengo maalum la kuhudumia vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuwasogeza vijana karibu na kuwapa fursa ya kutambua haki za vijana, afya, elimu, ulinzi wa watoto, na kuwawezesha kiuchumi.
Msaada huo umetolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Babawatoto kupitia mradi wa AHADI unaofadhiliwa na Serikali ya Canada (GAC).
Akizungumza wakati wa kukabidhi jengo hilo Mratibu wa Masuala ya Jinsi na Vijana Wizara ya Afya Gerald Kihwele amelipongeza shirika hilo na kusema kuwa uwepo wa huduma hiyo maalum kwa vijana itapelekea kuongezeka kwa idadi ya vijana wanaopata huduma za afya bora zaidi kutokana na kuwepo kwa usiri, faragha, mazingira tulivu, na mtazamo chanya kutoka kwa watoa huduma.
“Jengo hili litatumika kutoa huduma mbalimbali kwa vijana ikiwemo, elimu ya afya ya uzazi na ujinsia, ushauri na saha, tohara kwa vijana wa kiume, huduma za msongo wa mawazo na matumizi ya dawa za kulevya, upimaji wa afya,magonjwa ya zinaa na VVU, huduma baada ya mimba kuharibika, kupima mimba na huduma ya uzazi wa mpango, tiba ya magonjwa ya zinaa, ushauri wa afya ya akili, unyanyasaji wa kijinsia amesema Gerald Kihwele.
Akizungumza kwa Niaba ya Mganga Mfawidhi, Dkt Jumanne Mafele amesema kuwa jengo hilo litatumika kutoa huduma tatu ikiwemo huduma ya Damu Salama, Huduma za Vijana na Uzazi wa Mpango kwa kuwa huduma zote ni muhimu kwa vijana.
Kwa Upande wake Meneja wa Mradi wa AHADI Bw. Kasei Msuya amesema kuwa Utafiti unaonyesha kuwa vijana wengi hushindwa kufika vituoni kwa hofu ya kukosa faragha au kukutana na wahudumu wasio na lugha rafiki hivyo mradi umeboresha miundombinu hiyo ili kuondoa vikwazo hivyo na kuwafanya vijana wajisikie huru na wenye thamani.