24/10/2024
MISUKOSUKO
SURA YA KWANZA
Jakob Msafiri – kipande cha mwanaume, mrefu, mweusi na mkak**avu wa maungo, alisimama pembeni kimya akiungalia mlolongo wa wafungwa wenzake, katika gereza la Ngathi, wakati wakienda kupokea chakula chao.
Jakob alikuwa na ada ya kuzungumza machache na kufikiri mengi. Ingawa amekuwa katika gereza hili si zaidi ya miezi kumi sasa, amepata sifa au cheo cha mfungwa wa pekee – mfungwa ambaye hakusita kutumia nguvu zake katika kuwafunza adabu wale wote alioona wanamletea upumbavu bila kujali matokeo ya tabia hiyo.
Aghalabu ni wafungwa wachache sana ambao hufikia kuwa na sifa aliyokuwa nayo Jakob sasa, kwani k**a hawakufa kabla hawajapata sifa hiyo, wengi wao, k**a askari jela wengi walivyokuwa wakisema kwa utani, “nguvu za soda huwaishia’, wakatubu na kufuata amri k**a gereza lilivyowataka.
Kwa Jakob ilikuwa kinyume. Miezi minne ya mwanzo gerezani aliipitia katika purukushani na adhabu za kila aina – adhabu ambazo zilikuwa zimebuniwa na uongozi wa gereza kwa madhumuni mawili. Moja, kumtoa mkaidi anayejidai ameshindikana kiburi alichonacho na kumfanya atubu, au mbili, kumuua yule anayejifanya ni mkaidi wa kupindukia lakini hana nguvu na afya ya kutosha kuhimili adhabu hizo. Hata hivyo ni wachache waliokufa kwani wengi walitubu haraka. Jakob hakutubu wala hakufa. Vyovyote ilivyokuwa athari ya adhabu hizo ilikuwa ni kuongezeka kwa kiburi na jeuri aliyokuwa nayo.
Huenda Jakob alikuwa na bahati kwamba adhabu na purukushani alizokuwa akizipitia zilikoma ghafla miezi minne kamili tangu aingie gerezani hapo. Ni vigumu kutabiri kile ambacho kingetokea iwapo muda ambao Jakob angepitia hizi purukushani na adhabu ungezidi hiyo miezi minne. Angeweza akatubu, akafa au hata akaendelea kudumu katika tabia yake hiyo bila kuathirika.
Siku ambayo Jakob alitimiza miezi minne kamili tangu aingie gerezani aliamua kutoamka asubuhi k**a ilivyokuwa ada kwa wafungwa kila asubuhi; tayari kwa kuhesabiwa na kwenda kwenye sulubu mbali mbali. Matokeo yake ni kwamba wakati wa kuhesabiwa alikosekana hivyo ikabidi atafutwe. Kikundi cha askari jela kilichoingia alikokuwa analala kiliudhika vibaya sana baada ya kumkuta humo akiwa ameamka anafanya mazoezi mepesi ya viungo.
Baadhi ya wale askari jela walitaka kumvamia lakini kiongozi wao, mzee mmoja ambaye alikuwa na uzoefu wa muda mrefu sana k**a askari jela, aliwazuia akanong’ona.
“Hakuna haja. Ni kweli mtamk**ata na huenda mtafanikiwa kumvunja mkono, mguu au hata shingo, lakini ninavyohisi ni kwamba hajali. Zaidi ya hapo mmoja wenu au hata wawili ataishia vilevile na kutokuwa na meno au jicho au vyovyote. Nawajua sana viumbe wa aina yake.”
Walibaki wakimwangalia Jakob kwa muda ambaye hakuonyesha dalili yoyote ya kuwajali, kisha yule mzee akapaaza sauti na kusema.
“Mfungwa Jakob, hutakiwi kuwapo humu saa hizi.”
“Nafahamu”
Alijibu Jakob akaendelea na mazoezi yake.
“Sasa k**a unafahamu, mbona uko humu?”
“Nimeamua tu”. Alijibu Jakob, ghafla akaacha mambo aliyokuwa anafanya na kuwageukia.
“Nyie mbwa. Naona mna bunduki, kwa nini mmoja wenu asiitumie yake?.” Aliuliza kwa dharau.
“Hivyo ndivyo unavyotaka?”
“Ni dhahiri. Kwani huoni? Hiyo ndiyo njia pekee ambayo itakupungu*ieni kazi.” Alijibu Jakob.
Yule mzee alimkazia jakob macho kwa muda akatikisa kichwa.
“Hatuna haja ya kujipungu*ia kazi. Zaidi ya hayo, k**a una hamu sana ya kufa, kwa nini usijitundike?. Siyo jambo geni unajua? Ni jambo linalotendeka mara nyingi gerezani.”
Jakob alicheka.
“Nijitundike? Siwezi kujitundika. Mimi sio mwoga kiasi hicho.”
“Sawa Jakob, tumeshakusikia maoni yako. Lakini hatuhitajiwi kuendelea na soga hapa. Unachotakiwa kufanya ni kutoka humu na kwenda kazini k**a unavyopaswa.
Jakob alitikisa kichwa.
“Itabidi mnichukue na kwenda kuniadhibu k**a mnataka. Mtakuwa mnatimiza wajibu wenu. Unajua jana usiku wakati nimejilaza nilikuwa nawaza nini? ‘K**a kesho nisipokwenda kazini watakuja kunifuata humu. Tutaongea kwa muda lakini hatutaelewana.
Huenda mmoja wao akashawishika kunipiga risasi. Isipotokea hivyo itabidi wanichukue kwa nguvu, na katika harakati hizo virungu itabidi vitumike. Virungu vingi vinavyorushwa kwa pamoja, kimoja wapo, kwa bahati nzuri kinaweza kupiga kichwani chini ya kisogo, kwenye maungio ya shingo na kichwa……”
“Lazima ana wazimu!.” Alipayuka mmoja wa wale askari jela akikatiza kauli ya Jakob.
“Labda. Lakini sidhani. Ni mmoja wa wale wanafalsafa wasio na bahati.”
Alijibu kiongozi wa wale askari jela kisha akaendelea.
“Sawa Jakob. Kirungu kimoja chini ya kisogo, kwenye maungio ya shingo na kichwa, kitakuwa na athari ile ile ya kupigwa risasi ya moyo au kichwa. Nimekuelewa. Unaonaje tukifuatana kwenda ofisini?
“Ofisini? Tukafanye nini ofisini?.” Aliuliza Jakob uso wake ukionyesha kutatizwa.
“Ukweli ni kwamba sijui. Lakini vilevile ukweli ni kwamba kwa kuwa sasa najua nia yako, sitakupa furaha ya kuona risasi yoyote ikipigwa au virungu vyovyote vikipiga chini ya kisogo kwenye maungio ya kichwa na shingo. Tunakwenda au sisi tuondoke zetu?”
Jakob alisita kwa muda kisha akasema.
“Umeshazeeka. Hunda umeshafanya kazi hii kwa miaka ishirini au zaidi. Karibu utastaafu. Unajua unaweza ukafukuzwa kazi na kupoteza muda wako bure kwa kutofuata taratibu?”
“Miaka ishirini na mitano kazini. Nakaribia kustaafu. Naweza kufukuzwa kazi na kupoteza muda wangu, yote hayo ni kweli. Lakini, - lakini wewe siyo mwanafalsafa pekee asiye na bahati humu. Twende zetu.”
Jakob alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Sitapenda kukuona ukifukuzwa kazi. Lazima utakuwa na mke na watoto wanaokutegemea. Tunaweza tukakubaliana jambo moja. Mwanzoni ulinitaka niende kazini na haya mambo yaishilie mbali nikakataa. Unaonaje iwapo nitakwenda kazini leo k**a ulivyotaka, lakini na wewe kwa upande wako ukubali kwamba kesho au siku nyingine yeyote hutaongoza kundi lolote litakalotakiwa kunitafuta?”
“Hakuna makubaliano yoyote Jakob” alijibu yule kiongozi wa wale askari jela.
“Sawa. Wewe ni mtu mzuri lakini mjinga, k**a unadhani kufuatana na wewe kwenda ofisini itasaidia, twende.”
Dakika chache baadaye Jakob alikuwa akikabiliana na Mkuu wa Gereza. Walikuwa wako wenyewe wawili kwenye ofisi ya Mkuu huyo. Yule mzee askari jela aliyekuwa amemleta Jakob alikuwa ameamriwa na mkuu wake aondoke.
Mkuu wa gereza la Ngathi, Thomas Oringe, alikuwa ni mtu aliyepata umri wa miaka arobaini na mitano. Kulikuwa na minong’ono kwamba hakuipenda sana kazi yake, minong’ono ambayo ilizuka kutokana na kule kushindwa kwa juhudi zake za kubadilisha hali na mazingira ya magereza. Kushindwa kwa juhudi zake hakukuwa ni makosa yake. Mapendekezo yake mengi yalikuwa yamerudishwa na wakuu wake yakiwa yameambatana na taarifa fupi.
“Shukrani kwa mapendekezo yako, lakini tunasikitika kuwa hayazingatii hali halisi. Unalopendekeza ni sawa na kuligeuza gereza kuwa k**a shule au hospitali, hilo haliwezekani. Vilevile tutashukuru k**a hutatoa mapendekezo ya aina hiyo siku za baadaye”
Thomas Oringo, kiutaalam akiwa ni mwanasaikolojia aliyejigeuza askari aliendelea na juhudi zake kwa muda bila mafanikio na hatimaye ilibidi shauku aliyokuwa nayo itoweke kabisa baada ya kukumbushwa kuwa yeye alikuwa askari na ilimbidi aishi kwa ku*ingatia mila na desturi za kiaskari, k**a hazimfurahishi kwa nini asifungashe mizigo yake akaondoka?
Thomas Oringo hakufungasha akaondoka, lakini vilevile ilikuwa ndio mwisho wa juhudi zake. Walikuwepo watu wachache waliokijua kisa hiki cha Thomas. Kati ya hawa baadhi walimuona ni mjinga na wengine walimwonea huruma. Waliomuonea huruma walijua kuwa mbali ya juhudi zake nzuri kushindwa, alikuwa amewaudhi wakuu wake na kutokana na hali hiyo, asingetarajia cheo chochote zaidi ya kuishia na ukuu wa gereza.
Askari yule mzee aliyeongoza kikundi kilichomkuta Jakob akifanya mazoezi alifahamu kisa hiki cha Thomas Oringo na alikuwa miongoni mwa wale waliomuonea huruma. Hii ndiyo sababu iliyomfanya amwambie Jakob kuwa hakuwa mwanafalsafa pekee aliyekosa habati.
Thomas Oringo alimtaza Jakob kwa makini kwa muda mfupi kisha akamwashiria kiti kilichokuwa mbele ya meza yake.
“Keti tafadhali.” Alisema, akatoa paketi la sigara mfukoni akachomoa sigara mbili na kumkaribisha Jakob moja.
“Unavuta? Aliuliza.
Jakob aliketi akapokea sigara na kukubali kiberiti ambacho alikabidhiwa na Thomas.
“Kwa kawaida sivuti lakini gerezani unaweza ukafanya jambo lolote.” Alijibu Jakob akajiwashia sigara aliyopewa.
“Wakati mwingine ni kweli, wakati mwingine si kweli. Inategemea.” Alisema Thomas naye akajiwashia sigara yake.
“Kwa nini unasema wakati mwingine ni kweli na wakati mwingine si kweli.” Aliuliza Jakob.
“Nasema hivyo kwa sababu mabadiliko yanayompata mtu gerezani yanategemea kwa kiasi kikubwa mtizamo wa mtu mwenyewe. Tunachukulia tu kuwa magereza yanawabadilisha watu kwa sababu tunaona watu wengi wanaofungwa magerezani wakikumbwa na mabadiliko hayo. Lakini ni vizuri vilevile tukakumbuka kuwa watu walio wengi ni dhaifu na kwa kwa urahisi kabisa watajiachia wapate nafuu kidogo inayoambatana na mabadiliko ambayo mazingira yamelazimisha juu yao, hata k**a nafuu hiyo inaambata na kudhalilika na kujipotezea heshma. Wako watu wachache, tena wachache sana, ambao wako radhi kufa lakini wasiruhusu mabadiliko katika kile wanachokiamini.”
Thomas alinyamaza kwa muda akamkazia macho Jakob kisha akamnyooshea kidole cha shahada.
“K**a wewe Jakob. Unajaribu kujiua kwa sababu unaamini ndani ya tendo la kujiua na nimeshaona kuwa vyovyote tutakavyofanya hapa hutaacha kuamini hivyo. Wewe ni jasiri, na hilo hakuna mtu anayeweza kubisha; lakini kinachonishangaza ni kwamba ni kwanini hujaamua kujitundika?”
Jakob alivuta sigara yake kwa muda bila kujibu kisha akasema.
“Unajuaje kuwa nataka kujiua?”
“Wafungwa wote wenye tabia k**a yako napata taarifa zao na ku*ichunguza kwa makini. Tangu ufike hapa umekuwa ukitafuta kifo kwa nguvu sana lakini bahati imekuwa si yako. Bado nakuuliza. Kwa nini hujitundiki?.
“Sijitundiki kwa sababu, kufanya hivyo ni woga. K**a wewe ulivyo askari, na mimi kwa mtizamo wangu mwenyewe binafsi naamini kuwa ni askari. Napigana na yale yote ambayo katika mtazamo wangu naamini hayanifai. Situmaini kushinda, lakini kutokutumainia ushindi hakunifanyi niache kupagana. Nitaendelea kupigana mpaka atakapotokea mtu ambaye naye ana mtizamo wa aina yake aamue kunimalizia. Kwa mfano tu afande, wewe unaweza ukawa mtu k**a huyo. Hapo ulipo una bastola. Unaweza ukaichomoa na dakika chache baadaye nikawa marehemu. Utaandika ripoti k**a inavyotakiwa na kuelezea ilikuwaje n.k. huo ukawa ndiyo mwisho wa Jakob mwenye usumbufu.”
Fuata kiungo (link) hiki kuendelea kusoma hadithi hii ya kusisimua: https://wellbizsolutions.org/blog/f/misukosuko---sura-ya-kwanza