27/10/2014
Matumizi ya Dawa za Kulevya Yatakomeshwa!
“KOKEINI Nyingi Haramu Yapatikana Katika Chupa za Divai.” Makala moja ya gazeti iliyozungumzia kichwa hicho ilieleza jinsi polisi huko Johannesburg, Afrika Kusini, walivyopata kasha kubwa lenye chupa 11,600 za divai ya kutoka Amerika Kusini. Divai hiyo ilikuwa imechanganywa na kilogramu 150 hadi 180 za kokeini. Yaaminika kuwa hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha kokeini kuwahi kuingizwa nchini humo.
Ijapokuwa huenda ugunduzi huo ukaonyesha kwamba pambano dhidi ya dawa za kulevya linafaulu, ukweli ni kwamba polisi hupata asilimia 10 hadi 15 tu ya dawa haramu za kulevya ulimwenguni. Hilo linasikitisha kwa sababu ni sawa na mkulima anayekata majani machache ya gugu hatari linalomea haraka, na kuacha mizizi yake ardhini.
Jitihada za serikali za kukomesha utengenezaji na uuzaji wa dawa za kulevya huzuiwa na faida kubwa inayotokana na uuzaji wa dawa hizo. Inakadiriwa kwamba dawa za kulevya zenye thamani ya mabilioni ya dola zinauzwa na kununuliwa kila mwaka nchini Marekani peke yake. Kwa sababu ya pesa nyingi zinazohusika, si ajabu kwamba polisi na maofisa wa serikali, hata wale wenye vyeo vya juu, kutumbukia katika ufisadi.
Alex Bellos wa gazeti la The Guardian Weekly aliripoti kutoka Brazili kwamba uchunguzi mmoja wa bunge ulionyesha kwamba, “wabunge watatu, wasaidizi 12 wa serikali, na mameya watatu walitajwa . . . kwenye orodha yenye zaidi ya watu 800 ambao wanashukiwa kuhusika na uhalifu wa magenge na ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Brazili.” Orodha hiyo ilikuwa pia na majina ya “maofisa wa polisi, wanasheria, wafanyabiashara na wakulima kutoka majimbo 17 kati ya majimbo 27 nchini humo.” Profesa mmoja wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha Brasília alisema hivi: “Matokeo hayo yanaonyesha hali ya ujumla ya jamii nchini Brazili.” Ndivyo ilivyo katika jamii nyingi zinazokumbwa na matatizo makubwa ya dawa za kulevya. Sheria za uuzaji na ununuzi wa dawa za kulevya ndiyo inayoendeleza tatizo hilo.
Baadhi ya watu huteta ili dawa fulani za kulevya zihalalishwe kwa sababu wanajua kwamba vizuizi vya kisheria haviwezi kudhibiti dawa hizo. Kwa ujumla wanataka watu mmoja-mmoja waruhusiwe kuwa na kiasi kidogo cha dawa hizo kwa matumizi ya kibinafsi. Wanahisi kwamba hatua hiyo itasaidia serikali kudhibiti dawa hizo kwa urahisi na itapunguza faida kubwa za wafanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya.
Wengine Hufaulu
Mwanzoni huenda kumsaidia mraibu kuacha kutumia dawa za kulevya kukaboresha afya yake. Lakini inasikitisha kwamba mara tu mraibu arejeapo nyumbani, kuna uwezekano mkubwa wa kwamba huenda akashawishiwa kuanza tena kutumia dawa za kulevya. Mwandishi Luigi Zoja aeleza sababu: “Kumsaidia mgonjwa kuacha zoea fulani ni kazi bure iwapo hatasaidiwa kubadili kabisa njia yake ya kufikiri.”
Darren, aliyetajwa katika makala inayotangulia, alisitawisha ‘njia mpya ya kufikiri’ iliyobadili maisha yake. Aeleza hivi: “Mimi sikuamini kwamba Mungu yuko, lakini baada ya muda, niling’amua kwamba ni sharti Mungu awepo. Wakati huo nilikuwa mraibu wa dawa za kulevya. Kwa muda wa miezi miwili au mitatu, nilijaribu kuacha kutumia dawa za kulevya, lakini marafiki wangu hawakuniruhusu kuacha. Ingawa niliendelea kutumia dawa za kulevya, nilianza kusoma Biblia kwa ukawaida kabla ya kulala. Sikushirikiana na marafiki wangu mara nyingi. Jioni moja mimi na yule niliyeishi naye tulikuwa tumelewa kabisa baada ya kutumia dawa za kulevya. Nilimweleza kuhusu Biblia. Asubuhi iliyofuata alimpigia simu nduguye, ambaye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alituelekeza kwa Shahidi mmoja aliyeishi katika jiji letu, nami nikaenda kumwona.
“Kuacha uraibu wa dawa za kulevya si rahisi. Michael, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, afunua matatizo aliyopata alipoacha dawa za kulevya baada ya kuzitumia kwa miaka 11: “Nilikonda kwa sababu ya kushindwa kabisa kula. Nilihisi maumivu makali kana kwamba ninadungwa na sindano, nilitoka jasho, na kuona mazingaombwe. Nilitamani sana dawa za kulevya, lakini kujishughulisha na mambo ya kijamii kulinisaidia kuacha kabisa dawa za kulevya.” Watu hao waliokuwa wakitumia dawa za kulevya hapo awali wanakubali kwamba ilikuwa muhimu kwao kuachana kabisa na washiriki wao wa kale.