15/07/2025
Wakazi wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameguswa na taarifa ya kusikitisha kufuatia kifo cha Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Hospitali Teule ya Kibosho, Magreth Joseph Swai (30), aliyeripotiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia waya wa antena katika makazi yake yaliyopo Longuo, Kata ya Longuo, Tarafa ya Moshi Magharibi.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 10, 2025 majira ya saa tatu kamili usiku, ambapo marehemu alijinyonga kwa kutumia waya wa antena alioufunga kwenye nondo iliyopo juu ya mlango wa chumba chake.
“Chanzo cha tukio hili ni msongo wa mawazo uliosababishwa na matatizo ya afya ya akili. Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa marehemu alianza kuugua ugonjwa huo miaka minne iliyopita akiwa kwenye mafunzo kwa vitendo k**a daktari maalum wa watoto,” alisema SACP Maigwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu hakuwa akiishi na mtu mwingine nyumbani kwake na hakuacha ujumbe wowote wa maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo ya kusikitisha.
Tukio hili limekuja wakati jamii ikiendelea kukumbana na changamoto za afya ya akili miongoni mwa wataalamu wa sekta mbalimbali, likisisitiza umuhimu wa kuwapo kwa msaada wa kisaikolojia na huduma za ushauri nasaha katika maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.
Katika tukio lingine la kusikitisha, Mfanyabiashara mkazi wa Msaranga, Ronald Malisa (35), naye ameripotiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka bafuni kwake siku hiyo hiyo ya Julai 10, 2025.
Taarifa zinaeleza kuwa Ronald alikuwa amefunga ndoa miezi minane tu iliyopita, lakini sababu za kuchukua uamuzi huo hazijafahamika hadi sasa.
Kamanda Maigwa amesema uchunguzi wa awali unaendelea huku mazishi ya Ronald yakitarajiwa kufanyika Julai 15, 2025 katika makaburi ya familia.
Mfululizo wa matukio haya ya kujiua umeibua hisia mseto katika jamii, huku wengi wakitoa wito kwa Serikali na wadau wa afya kuimarisha huduma za ushauri nasaha, hasa kwa vijana na wataalamu wanaokabiliwa na msongo wa mawazo.
Aidha, jamii inahimizwa kushirikiana kwa karibu na watu wanaoonesha dalili za matatizo ya kiakili kwa kuwasaidia kupata msaada wa kitabibu mapema.