
19/07/2025
MOI YAENDELEA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WAGONJWA
Na Amani Nsello- MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa wa dharura bila kuhitaji malipo ya awali, ikiwa ni sehemu ya kujali maisha ya wagonjwa na kutekeleza wajibu wake wa kutoa huduma bora za afya kwa jamii.
Hayo yalibainishwa jana Julai 18, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mapato wa MOI, Bw. Chediel Mziray wakati akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa ambapo amesema kuwa taasisi hiyo ina utaratibu wa kumhudumia mgonjwa wa dharura haraka iwezekanavyo bila kuzuia huduma kwa sababu ya malipo.
"Kwa wagonjwa wa dharura, MOI hatuzuii huduma kwa sababu ya fedha... Tunatoa huduma kwanza, malipo hufuata baadae. Kipaumbele ni kuokoa maisha ya mgonjwa. Baada ya mgonjwa kuwa katika hali tulivu, ndipo hatua za malipo hufuata kwa utaratibu rasmi wa taasisi" alisema Bw. Chediel na kuongezea
"Huu ni utaratibu uliowekwa mahsusi kusaidia kuokoa maisha na kuondoa mzigo kwa wananchi wakati wa dharura”
Aidha, alieleza kuwa mfumo huo unazingatia misingi ya utu, usawa na haki ya kila mtu kupata huduma za afya bila kujali hali yake ya kiuchumi wakati wa dharura.
Kwa upande wake, Ernest Mgogo, mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa ndugu wa mgonjwa aliwapongeza watumishi wa MOI kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo wao wa kujitolea kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura hususani wa ajali za barabarani.
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake imetenga siku ya Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kusikiliza maoni, kero, changamoto na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo.