
28/12/2024
MAJIBU YA URINALYSIS( *UCHAMBUZI WA MKOJO* ) YENYE VIASHIRIA VYA CHANGAMOTO YA FIGO.
Urinalysis ni kipimo cha uchunguzi wa mkojo kinachofanywa kwa lengo la kubaini changamoto mbalimbali za kiafya. Mara nyingi Urinalysis hufanywa kwa ajili ya kubaini maambukizi katika njia ya mkojo yaani UTI. Hata hivyo Urinalysis ni kipimo kinachoweza kutoa taswira kuhusu matatizo mengine ya kiafya ikiwemo changamoto ya figo.
Kutokana na urinalysis kuweza kubaini changamoto za afya ya figo, kuna baadhi ya wataalam kipimo hiki hukiita "poor person's kidney biopsy" yaani "biopsia ya figo ya mtu masikini". Uchunguzi wa biopsia ni uchunguzi ambao huhusisha kuchukua kipande kidogo cha sehemu ya ogani (tishu) na kwenda kuchunguzwa maabara ili kubaini changamoto za kiafya katika ogani hiyo. Kwahiyo urinalysis huitwa biospsia ya figo ya mtu masikini kwasababu ni kipimo cha gharama ndogo kinachoweza kueleza taarifa nyingi za afya ya figo bila kutumia tishu kutoka kwenye figo yenyewe.
Majibu ya urinalysis yanayoweza kuonyesha viashiria vya changamoto ya figo ni pamoja na yafuatayo;
1. Uwepo wa Protini (Proteinuria): uwepo wa protini kwenye mkojo kunaweza kuashiria athari kwenye glomeruli sehemu ya figo ambayo huchuja damu. Pia mkojo wenye protini Kwa wingi ukiutazama hata kwa macho utaweza kuuona ukiwa na povu jingi.
2. Chembchembe nyekundu za damu (RBCs)-Uwepo wa RBCs unaweza kuashiria athari kwenye figo kitu kinachofanya RBCs kupenya na kuingia kwenye mkojo. Hata hivyo RBCs kwenye mkojo zinaweza kuletwa na sababu nyingine k**a vile majeraha kwenye njia ya mkojo hasa kibofu au maambukizi mfano kichocho na UTI ya juu.
3. Low specific gravity- Specific gravity ni kipimo cha kukolea kwa mkojo (urine concentration) kiwango cha kawaida cha specific gravity ya mkojo ni kuanzia 1.005 mpaka 1.030. Mkojo wenye specific gravity chini ya 1.005 unaweza kuashiria changamoto katika uchujaji wa figo, hata hivyo Low specific gravity ya mkojo inaweza kuchangiwa na sababu nyingine k**a vile kunywa maji kwa wingi, matumizi ya baadhi ya dawa, n.k
4. Uwepo wa Casts: Casts huwa ni mkusanyiko wa Protini au cells zilizotengeneza umbo la silinda hiki ni kiashiria kuwa zimetoka kwenye tyubu ndogondogo zilizomo kwenye figo, Kuna RBCs casts, WBCs casts, Granular casts, n.k. Uwepo wa casts hizi huashiria changamoto kwenye figo hasa uwepo wa Granular casts ndiyo huashiria dalili za uharibifu sugu wa figo.
5. pH isiyo ya kawaida- kwa kawaida pH ya mkojo huanzia 4.5 mpaka 8.0. pH chini ya hapo au juu ya hapo inaweza kuashiria changamoto kwenye figo/mfumo wa mkojo, changamoto hiyo inaweza kuwa ni UTI au changamoto nyingine ya kiafya ikiwemo magonjwa sugu ya figo.
- Hata hivyo, majibu yote haya yanaonyesha viashiria tu, kupitia majibu haya unaweza kuanzisha uchunguzi wa vipimo maalum kwa ajili ya kuangalia ufanyaji kazi wa figo k**a vile Serum creatinine, Blood Urea Nitrogen, Urine Albumin Creatinine Ratio (uACR) n.k.
- Kupata dondoo muhimu za afya kila siku, nifuatilie kupitia mitandao ya kijamii;
- Instagram: Dr.Avneenfx
- Facebook: Uzazi Salama na Dr Avneen
- X(Twitter) Avneen
- TikTok Avneen