23/12/2025
Viongozi na wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Consolata Ikonda, wametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe leo Desemba 23, 2025 na kujionea hali ya utoaji Huduma katika jengo la Huduma za Afya ya Mama na Mtoto ambapo pia wamepata wasaa wa kubadilishana uzoefu na kushauriana na wataalamu wenyeji katika maeneo hayo.
Timu ya wataalamu hao imeongozwa na Elide Ambrositte ambaye aliongozana na Timu ya Wauguzi, na Madaktari kutoka Hospitali hiyo iliyopo wilaya ya Makete.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Edward Mhina, amepongeza uamuzi uliofanywa na wataalamu hao huku akiahidi pia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kuendeleza ushirikiano ambao umekuwepo na Hospitali ya Ikonda, hasa katika maeneo ya kujengeana uwezo, kushiriki uzoefu ili kuendelea kuboresha hali ya utoaji huduma za afya kwa watanzania.
Kiongozi wa msafara huo wa wataalamu kutoka Ikonda, Bi. Ambrositte, amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika eneo la Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, ikiwemo wataalamu wa kutosha na miundombinu ya kisasa k**a vile vifaa na dawa; ambapo amesisitiza ipo haja kubwa ya kuendeleza ushirikiano miongoni mwa wataalamu ili kujengeana ujuzi na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi hizo mbili.