18/08/2020
Kumbemenda mtoto ni nadharia inayomaanisha kudhoofika kwa afya ya mtoto wakati wa siku za mwanzo kabisa za matumizi ya ziwa la mama yake.
Hudhaniwa kutokana na mama kushiriki tendo la ndoa na mmewe au hata kutoka nje ya ndoa wakati bado ananyonyesha.Imani hii huenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa shahawa au mbegu za kiume zinazomwagwa wakati wa tendo la ndoa huingia na kuchanganyikana na maziwa ya mama ambayo baadae hunyonywa na mtoto hivyo kusababisha hali ya kubemendwa kwa mtoto
UKWELI NI UPI?
Haya ni madai ya uongo kwa 100% na hayana hata chembe ya ukweli.Shahawa/manii au hata mbegu za kiume zinazotolewa wakati wa tendo la ndoa huishia safari yake kwenye tumbo la uzazi na huharibiwa huko.Haziwezi kuingia kwenye mfumo wa mzunguko wa damu mwilini hivyo hakuna namna zitaingilia uzalishwaji wa maziwa ya mama
LINI MWANAMKE AFANYE MAPENZI BAADA YA KUJIFUNGUA?
Tendo hili mara nyingi hushauriwa lifanyike wiki 6 baada ya kujifungua.Linaweza pia kufanyika hata baada ya wiki 4 ikiwa tu uchafu na majimaji yenye damu yanayotolewa na mama kupitia uke yatakoma.Tendo hili hutegemea utayari wa mama,uwezo wake katika kulihimili na kasi ya kupona kwa vidonda na mipasuko aliyoipata wakati wa kujifungua.
MUHIMU
Kubemendwa kwa mtoto hakuna uhusiano wowote na kufanya mapenzi.Ukiona afya ya mwanao inadhoofika ni lazima atakuwa na matatizo ya kiafya,au hata hapati matunzo na virutubisho vya kutosha.Inaweza ikawa sababu hapati maziwa ya mama ya kutosha,hanyonyi vizuri,kuanzishiwa vyakula vya ziada mapema hasa kabla ya miezi 6 ya mwanzo,homa za mara kwa mara,nimonia,UTI pamoja na matatizo mengine mengi.Ni vyema akapelekwa hospitalini mapema ili asaidiwe kuliko kuendelea na dhana POTOFU ya kusingizia kuwa tendo la ndoa ndiyo chanzo.
Ukiwa na swali uliza